Serikali
imewataka wananchi kujihadhari na wizi ambao hufanywa na Taasisi
za Fedha hewa ambazo zimekuwa zikidai kutoa mikopo kwa njia ya simu.
Tahadhari
hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Assah
Mwambene wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Amesema
kuwa Taasisi hizo zimekuwa zikitumia mitandao ya simu za mkononi
kutapeli wananchi kwa kuwaraghai kuwa watawapatia mikopo.
Mwambene
ameongeza kuwa Taasisi hizo zimekuwa zikitumia majina ya viongozi
wakubwa mbalimbali wa vyama na Serikali kuwatapeli wananchi kwa
kuwachukulia fedha zao.
Amesema kuwa baadhi ya taasisi hizo zinatumia namba za uongo za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwaibia wananchi.
Mkurugenzi
huyo amezitaja baadhi ya Taasisi hizo kuwa ni pamoja na Social credit
Loans ambayo inadai imesajiliwa na TRA kwa namba Reg.No.33/SCC/REG/7894
na namba ya utambulisho wa mlipa kodi ni TIN:203-344-6789.
Taasisi nyingine ni Saving Foundation na Quicken Loan ambazo zote hizo zimekuwa zinawatapeli wananchi.
Amesema kuwa baada ya kuwasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania, imebainika kuwa hakuna taarifa yoyote kuhusu Taasisi hizo.
Mwambene amesema kuwa Serikali inaendelea kufanyia uchunguzi ili wahusika waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua.
Aidha ,
Mkurugenzi huyo amewakumbusha wananchi kutokubali maombi ya fedha,
fadhila au maelekezo yanayodaiwa kutolewa na uongozi wa juu bila kupata
uthibitisho kutoka mamlaka husika.