Inawezekana likawa jambo nadra kutokea kwa sasa, lakini enzi za uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere lilitokea.
Ni baada ya mwasisi huyo wa Taifa kuamua kwa hiari
kupunguza mshahara wake kwa asilimia 10 ili kupunguza pengo baina ya
maskini na wale wenye kipato cha juu, uamuzi ambao ulifuatwa na
aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati huo, Edwin Mtei.
Mwaka 1968, Mwalimu Nyerere aliyekuwa akilipwa
mshahara wa Sh5,000 kwa mwezi alikiona ni kiasi kikubwa ikilinganishwa
na wengi wa watumishi na hivyo kuamua kukipunguza.
Mshahara huo wa Mwalimu Nyerere ni sawa na ambao
alikuwa akilipwa pia Gavana Mtei. Kutokana na punguzo hilo, mishahara
yao ilishuka hadi Sh4,500 kwa mwezi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi
hili nyumbani kwake Tengeru, nje kidogo ya Mji wa Arusha Jumatatu
iliyopita, Mtei alisema alifikia uamuzi huo wa kupunguza mshahara wake
baada ya Mwalimu Nyerere kutangaza kupunguza mshahara wake.
Alisema: “Nilipunguza mshahara wangu tena kwa hiari yangu baada ya kuona Mwalimu Nyerere amepunguza wa kwake.”
Alisema wakati ule mshahara wa Gavana ulikuwa
ukipangwa na Serikali na kwamba ulikuwa na kipengele katika mkataba
kikionyesha kuwa hauwezi kupunguzwa na mamlaka yoyote, labda atakapotaka
mwenyewe.
Mtei ambaye pia ni mwasisi wa Chadema alisema
sababu nyingine iliyomsukuma kupunguza mshahara wake ni kuona kwamba
kama asingefanya hivyo, basi angemzidi mshahara Rais (Nyerere), kitu
ambacho kwake hakukipenda.
Alisema, ingawa Mwalimu Nyerere alipunguza
mshahara, lakini yeye kisheria hakuwa akibanwa kufanya hivyo kutokana na
mkataba wake ambao ulikuwa ukiibana Serikali kutokuugusa mshahara wake.
Alieleza kuwa ukimwondoa yeye na Mwalimu Nyerere,
Serikali iliamua kuwapunguzia mishahara watumishi wengine wa kada
nyingine serikalini ili kubana matumizi.
“Watu wote walipunguziwa mishahara kuanzia vigogo
wote (wa wakati ule),” alisema Mtei ambaye Jumamosi iliyopita alitimiza
miaka 82 tangu kuzaliwa kwake.
Sababu za punguzo hilo
Alisema Serikali ya Mwalimu Nyerere iliamua kuchukua hatua hiyo
baada ya kuona kuwa kulikuwa na pengo kubwa la kipato kati ya watumishi
wa ngazi za chini na wale wa juu.
Mwanasiasa huyo ambaye aliteuliwa kuwa Gavana wa
BoT akiwa na umri wa miaka 32, jambo ambalo ni mara chache kufanyika kwa
vijana kuaminiwa na hata kupewa madaraka makubwa kiasi kile, alisema
Mwalimu Nyerere alimwamini kwa kiasi kikubwa.
Kuhusu Mwalimu Nyerere, Mtei alisema alikuwa
kiongozi mwadilifu, ndiyo maana akafanya uamuzi mgumu kama huo wa kugusa
mshahara wake mwenyewe.
Alisema kwa kizazi cha sasa ni watumishi wachache wa kuweza kuwalinganisha naye.
Alisema baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka katika
uongozi wa nchi, watumishi na hata viongozi walibadilika na kujiingiza
katika mambo mengi yakiwamo yale ambayo yanakwenda kinyume na maadili.
Uongozi wa sasa
Mtei ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Fedha kabla ya kuteuliwa kuwa Gavana wa BoT alisema katika mazingira
ya sasa hakuna kiongozi yeyote ambaye anaweza kukubali au kupunguza
mshahara wake.
“Katika mazingira ya sasa, jambo hilo haliwezekani
kabisa,” alisema. Aliongeza: “Hivi sasa viongozi wengi wanashindana
kupeleka na kuficha fedha Uswisi, wengi wao wanakimbilia kwenye utajiri,
si utumishi.”
Alisema hivi sasa viongozi wengi wametanguliza
mbele masilahi yao na wengine kujiingiza kwenye ufisadi na hivyo
kushindwa kuwatumikia wananchi ipasavyo.
Mtei alisema viongozi wote lazima waongozwe na uzalendo na kuwahurumia wananchi wengi ambao ni maskini.
Alisema uamuzi walioufanya yeye na Mwalimu Nyerere
hivi sasa unaweza kufanyika katika chama kingine kinachojali wananchi
endapo kitaingia madarakani, ambacho hata hivyo alisema siyo CCM.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi