Jaji wa Mahakama Kuu, Grace Mwakipesile amefungua kesi ya madai ya kulipwa fidia ya Sh milioni 300 kutokana na majeraha na maumivu aliyoyapata katika ajali aliyoipata mkoani Shinyanga.
Amefungua
kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya dereva Kamota
Hassan, Michael Mosha na kampuni ya bima ya Zanzibar. Kesi hiyo
itatajwa Agosti 4 mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa.
Katika
hati ya madai, Jaji Grace anaiomba mahakama iamuru walalamikiwa hao
wamlipe fedha hizo kutokana na ajali anayodai ilitokana na uzembe wa
dereva Hassan aliyekuwa anaendesha gari aina ya Mitsubishi Fuso lenye
namba za usajili T 683 AKN, iliyokuwa imewekewa bima na kampuni ya
Zanzibar.
Inadaiwa
Septemba 17 mwaka 2011 katika kijiji cha Bubihi, Wilaya ya Kishapu,
mkoani Shinyanga, Jaji Grace akiwa abiria kwenye gari aina ya Toyota
Landcruiser lenye namba za usajili STJ 1870 likiendeshwa na Mosha,
waligongwa na Fuso hilo.
Anadai
kutokana na ajali hiyo alipata maumivu na majeraha katika sehemu
mbalimbali za mwili na kupelekwa katika hospitali ya mkoa ya Shinyanga
ambapo alipata matibabu na kuhamishiwa Taasisi ya Mifupa, Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (MOI) ambapo aliendelea na matibabu ya nje kwa miezi
sita.