KAMPUNI ya Uwindaji wa Kitalii,
Green Miles Safaris ya nchini imenyimwa kibali maalumu cha uwindaji huo kwa
kuzingatia sababu zinazodaiwa si sahihi, uamuzi uliosababisha wawindaji
mashuhuri kutoka familia ya kifalme huko Umoja wa Falme za Kiarabu kufuta safari
yake ya kuja kuwinda nchini na hivyo, nchi kupoteza mabilioni ya fedha kwa njia
ya mapato.
Hali hiyo inahusishwa na utendaji
kazi wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, unaodaiwa na baadhi ya
watendaji wizarani kwake kwamba unaendelea kuigharimu Serikali ambapo katika
suala la uwindaji wa kitalii anatajwa kuwa na mgongano wa kimaslahi kati yake
na moja ya kampuni za uwindaji dhidi ya nyingine, akishindwa kuchukua hatua
muhimu kwa kadiri anavyoshauriwa na baadhi ya watendaji wake waandamizi wizarani.
Gazeti hili katika uchunguzi wake
unaothibitishwa na nyaraka mbalimbali, limebaini mtego uliotegeshwa dhidi ya
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kutokana na mgongano wa
kimaslahi na kampuni binafsi za uwindaji wa kitalii, ndani ya Wizara ya
Maliasili na Utalii.
Ni katikati mgogoro huo, taarifa
za uhakika zinabainisha kwamba Tanzania itapoteza mabilioni ya fedha
yaliyopaswa kukusanywa kutokana na wawindaji wakubwa kutoka nchi za Falme za
Kiarabu, baada ya kampuni yenye kuaminika na ukanda huo kunyimwa kibali maalumu
cha uwindaji.
Kiini cha mgogoro
Kwa mujibu wa nyaraka kadhaa,
Waziri Nyalandu anadaiwa kuchelewa kutoa uamuzi unaoiumiza kampuni ya uwindaji
ya Marekani, Wengert Windrose Safaris (WWS) dhidi ya kampuni ya Tanzania, Green
Mile Safaris Ltd.
Kati ya mizozo iliyopo baina ya
kampuni hizo msingi wake ni uamuzi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, mwaka
2011, kugawa vitalu vya utalii kwa wadau wake kwa ajili ya kipindi cha mwaka
2013-2018.
Katika uamuzi huo wa ugawaji wa
vitalu, vitalu vya uwindaji vya Pori Tengefu Lake Natron ambavyo ni Lake Natron
GCA Kaskazini-Kusini cha daraja la II na Lake Natron GCA Kaskazini cha daraja
la kwanza, vilivyotokana na kugawanywa kwa kitalu kimoja cha Lake Natron GCA
North kilichokuwa kikimilikiwa na Wengert Windrose Safaris (WWS).
Ni kutokana na mgogoro huo, hatua
mbalimbali zilichukuliwa ambazo hazikuiridhisha WWS iliyochukua uamuzi wa
kuiomba Mahakama kutoa amri ya siku 90 kutoruhusu shughuli zozote kufanyika,
amri ambayo ilitolewa Mei 29 hadi Septemba 2013, ilipokwisha muda wake, na
hivyo kupaswa kuiacha huru kampuni ya Kitanzania ya Green Miles Safaris kufanya
shughuli zake.
Taarifa zinabainisha kwamba baada
ya Septemba 30, mwaka jana, WWS hata hivyo walifungua kesi wakiomba Mahakama
izuie wao kuondoka kwenye kitalu ambacho hawakuwa na uhalali nacho, wakitaka
waruhusiwe kuwinda kwenye kitalu hicho cha Lake Natron GCA East.
Hata hivyo, Mahakama ilitupilia
mbali maombi hayo kwa kuweka bayana hayakuwa na msingi na kuhusu ombi lao la
kutaka kuruhusiwa kuwinda Mahakama iliweka bayana haina mamlaka ya kutoa vibali
vya uwindaji.
Nyalandu akalia ushauri
Kutokana na mlolongo mrefu wa
suala hilo, sambamba na ushauri wa baadhi ya watalaamu wa Wizara ya Maliasili
na Utalii, inadaiwa kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii, Nyalandu amebaki
kimya kutoa uamuzi unaoitendea haki Kampuni ya Green Mile Safaris inayofanyiwa
fujo na kampuni ya WWS.
Ushauri huo umetolewa kwa
kuzingatia Sheria ya Wanyamapori na Kanuni za Uwindaji wa Kitalii. Kwa kupuuzia
kutoa uamuzi, Waziri Nyalandu anadaiwa kuweza kuisababishia gharama zisizo na
lazima Serikali.
Serikali kukosa mabilioni
Mgogoro huo kwa kiasi fulani pia,
kwa misingi ya upotoshaji unadaiwa kuiponza Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, inayoongozwa na Waziri Bernard Membe, ambayo kupitia
kwa barua yake ya Juni 12, mwaka huu, iliuandikia Ubalozi wa Falme za Kiarabu
Tanzania, kueleza ni kwa sababu zipi, Kampuni ya Green Miles Safaris inayopaswa
kupokea wageni mashuhuri kutoka nchi hizo wanayimwa kibali maalumu cha
uwindaji.
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, kutokana na ushawishi wa Wizara ya Maliasili na
Utalii, nayo ilibainisha sababu kuu mbili za kutokutoa kibali maalumu cha
uwindaji.
Kati ya sababu hizo; mosi ni
suala la kitalu cha Lake Natron ambako wageni hao mashuhuri kutoka Falme za
Kiarabu wanataka kwenda kufanya uwindaji wa kitalii, mzozo wake unafanyiwa kazi
na Mahakama na kwa hiyo, kutoa kibali ni kuingilia mhimili wa Mahakama.
Hata hivyo, udhaifu wa sababu
hiyo ya kwanza, kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya sheria ambao majina yao
yanahifadhiwa kwa sasa, ni kwamba kilichopo mahakamani si zuio (injuction) kwa
Kampuni ya Green Miles Safiris kuendesha shughuli zake, bali ni mchakato wa
kawaida wa kimahakama.
Sababu nyingine ya pili
iliyoanishwa na Wizara ya Mambo ya Nje kwa ubalozi wa United Arab Emirate,
jijini Dar es Salaam ni kampuni ya Green Miles Safaris kuwa chini ya uchunguzi
wa Bunge.
Vile vile, kwa kuzingatia
utaalamu wa kisheria, gazeti hili limedokezwa kwamba uchunguzi wowote wa
kibunge hauwezi kuzuia shughuli za kiserikali kuendelea, ikiwamo shughuli ya
utoaji kibali maalumu kwa Green Miles Safaris, hasa pale ambapo mapato ya
mabilioni kwa nchi yanapokuwa hatarini kupotea.