WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la kujenga
Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na
Jumuiya ya Kimataifa kutoa ushirikiano wa ulinzi na amani katika mataifa
yenye matatizo ya amani.
Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam jana,
wakati akizindua Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi na Amani, kilichojengwa kwa
msaada wa Serikali ya Canada na kulenga kutoa mafunzo maalumu kwa
maofisa wa Jeshi wa kulinda amani katika nchi zenye matatizo ya amani.
Alisema mafunzo yatakayotolewa na chuo hicho yatasaidia kupunguza
madhara ya ushambuliwaji wa wanajeshi watakaoshiriki katika ulinzi wa
kulinda amani katika mataifa hayo.
“Chuo hicho kitakuwa kikipokea wanafunzi
watakaopata mafunzo haya kutoka nchi mbalimbali zilizopo katika Jumuiya
ya Kimataifa, zikiwemo Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Darfur –
Sudan, ambazo tumekuwa tukishiriki kupeleka wanajeshi wetu wa kulinda
amani na usalama katika mataifa yao. “Mafunzo yatakayotolewa katika chuo
hicho yatahusiana na mbinu zote za kiusalama na amani kwa wanajeshi wa
kulinda amani, ambao watakuwa wakijifunza jinsi ya kukabiliana na hatari
pindi wawapo katika majukumu yao.
“Kutokana na mafunzo watakayoyapata,
tunaamini hata madhara ya wanajeshi wetu waliokuwa wakienda kulinda
katika nchi hizo yatapungua, kwani watakuwa na ujuzi zaidi, ikiwa ni
pamoja na mbinu za kujilinda dhidi ya adui,” alisema Dk. Mwinyi. Alisema
kutokana na uwepo wa chuo hicho nchini, amewataka wanajeshi wa kulinda
amani kuitumia fursa hiyo katika kujiimarisha kimbinu na fikra ili
waweze kupata uzoefu wa kutosha kabla ya kuingia eneo la vita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi na Usalama Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema
wakufunzi wa mafunzo yatakayotolewa watatoka hapa nchini pamoja na
baadhi ya mataifa rafiki wanaoshirikiana kutoa ulinzi na amani katika
mataifa hayo. Alisema chuo hicho kimelenga kuanza kuchukua wanafunzi 70
watakaojifunza mafunzo hayo kulingana na aina ya masomo watakayochukua.
Alisema katika kuepusha mwingilianao baina ya wananchi na chuo hicho,
Jeshi limekusudia kuanza ujenzi wa wigo utakaowatenganisha ili kuepusha
migogoro ya mwingiliano wa ardhi.
“Nawaomba wote watakaopata nafasi ya
kujifunza mafunzo haya wawe makini na kutumia fursa hii katika
kujiimarisha kimbinu, kwani itawasaidia pindi watakapokuwa katika eneo
hatarishi kuweza kuchukua uamuzi sahihi wa kukabiliana na adui,” alisema
Jenerali Mwamunyange.